TARI, CBT yatoa mafunzo ya viuatilifu kwa maafisa ugani

 

Mtaalamu wa uthibiti wa visumbufu vya mazao kutoka TARI Naliendele,Stanslaus Lilay akifundisha jinsi ya kutambua magonjwa ya mikorosho na tiba zake kwa maafisa ugani

Haya ni mafunzo yanayotolewa kwa maafisa ugani yanayohusu matumizi sahihi na salama ya viuatilifu ili waweze kutoa elimu kwa wakulima wa zao la korosho lengo likiwa kufikia uzalisha mzuri wa zao hilo

NA Musa Mtepa

Zaidi ya maafisa ugani 500 kutoka mkoa wa Mtwara watanufaika na mafunzo maalum ya matumizi sahihi na salama ya viuatilifu vya zao la korosho, pamoja na mbinu bora za kuchanganya viuatilifu hivyo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo muhimu la biashara.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele, ambapo June 5,2025 yamefanyika katika mtaa wa Mbawala Chini, Manispaa ya Mtwara-Mikindani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo, Mshauri wa Kilimo Mkoa wa Mtwara, Ally Linjenje, amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo maafisa ugani 323 kutoka halmashauri tisa za mkoa wa Mtwara pamoja na maafisa ugani 245 waliopo chini ya Bodi ya Korosho kupitia mpango wa BBT.

Sauti ya Ally Linjenje – Mshauri wa Kilimo Mkoa wa Mtwara

Kwa upande wake, Stanslaus Lilay, mtaalamu wa uthibiti wa visumbufu vya mazao kutoka TARI Naliendele, amesema kuwa serikali inalenga kufikia uzalishaji wa tani 700,000 za korosho ifikapo mwaka 2026. Ili kufanikisha hilo, elimu ya matumizi sahihi ya viuatilifu inapaswa kuwafikia wakulima kupitia maafisa ugani waliopatiwa mafunzo ya kitaalamu.

Sauti ya Stanslaus Lilay – TARI Naliendele (Sauti ya 1)

Aidha, Lilay ameongeza kuwa pamoja na matumizi sahihi ya viuatilifu, maafisa ugani wanapaswa pia kuwasaidia wakulima kutambua visumbufu vikuu vya zao la korosho kama vile ubwiri unga, braiti na dieback ili waweze kukabiliana navyo mapema.

Sauti ya 2 – Stanslaus Lilay

Geofrey Mwalembe, Afisa Kilimo Mwandamizi kutoka CBT, amebainisha kuwa kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2025/26, serikali inatarajia kuwafikia maafisa ugani zaidi ya 500 kwa mkoa wa Mtwara pekee. Mafunzo haya yataanza kwa awamu ya kwanza katika mikoa ya Lindi na Mtwara kabla ya kusambaa maeneo mengine.

Sauti ya Geofrey Mwalembe – Afisa Kilimo Mwandamizi, CBT

Kwa upande wao, maafisa ugani na wakulima walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo, wakisisitiza kuwa yana manufaa makubwa kwao na kwa wakulima, huku wakiiomba serikali kuhakikisha mafunzo haya yanaendelea kufanyika mara kwa mara ili kuleta matokeo chanya katika uzalishaji wa korosho.

Sauti ya baadhi ya maafisa ugani na wakulima

Comments