
Haya ni mafunzo yanayotarajiwa kuwafikia zaidi ya maafisa ugani 500 katika mkoa wa Mtwara ambapo kwa hatua ya awali yanatarajiwa kufanyika katika mikoa yaLindi na Mtwara
NA Musa Mtepa
Zaidi ya maafisa ugani 500 kutoka mkoa wa Mtwara watanufaika na mafunzo maalum ya matumizi sahihi na salama ya viuatilifu vya zao la korosho, pamoja na mbinu bora za kuchanganya viuatilifu hivyo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo muhimu la biashara.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele, ambapo June 5,2025 yamefanyika katika mtaa wa Mbawala Chini, Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa TARI Naliendele, Bakari Kidunda, mtaalamu wa utafiti kutoka taasisi hiyo, amesema kuwa mabadiliko ya uzalishaji wa korosho kwa miaka ya hivi karibuni yamesababishwa na changamoto kadhaa zikiwemo utambuzi na udhibiti hafifu wa magonjwa na wadudu waharibifu wa zao hilo
Aidha Bakari kidunda amesema pamoja na lengo kuu la mafunzo hayo kuwa na matumizi sahihi na salama ya viuatilifu lakini pia amewataka maafisa ugani kuwa na mawasiliano ya karibu baina ya watafiti na wakulima ili kuweza kuzifahamu na kuzifikisha kwa uharaka changamoto zinazojitokeza katika zao la Korosho.
Kwa upande wake, Stanslaus Lilai, mtaalamu wa uthibiti wa visumbufu vya mazao kutoka TARI Naliendele, amesema kuwa serikali inalenga kufikia uzalishaji wa tani 700,000 za korosho ifikapo mwaka 2026. Ili kufanikisha hilo, elimu ya matumizi sahihi ya viuatilifu inapaswa kuwafikia wakulima kupitia maafisa ugani waliopatiwa mafunzo ya kitaalamu.

Aidha, Lilai ameongeza kuwa pamoja na matumizi sahihi ya viuatilifu, maafisa ugani wanapaswa pia kuwasaidia wakulima kutambua visumbufu vikuu vya zao la korosho kama vile ubwiri unga, braiti na dieback ili waweze kukabiliana navyo mapema.
Kwa upande wao, maafisa ugani na wakulima walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo, wakisisitiza kuwa yana manufaa makubwa kwao na kwa wakulima, huku wakiiomba serikali kuhakikisha mafunzo haya yanaendelea kufanyika mara kwa mara ili kuleta matokeo chanya katika uzalishaji wa korosho.
Comments
Post a Comment